51. Idadi Ambayo Kwayo Yakini Hutokea
51. The Number By Which The Certainty Occurs
Kuna mvutano kuhusu idadi ndogo kabisa ambayo yakini hutokea. Baadhi walisema: tano; wengine walisema: idadi ndogo ni kumi na mbili; baadhi yao walisema: idadi ndogo ni ishirini; wengine walisema: ni arobaini; wengine walisema: sabini; na wengine walisema: ni mia tatu na kumi na tatu, na kadhalika. Kauli hizi zote zinazobainisha idadi maalum hazina msingi wa kinukuu wala wa kiakili, kwa kuwa hakuna dalili ya maandiko iliyokuja na idadi maalum, wala akili haiipendelei idadi maalum. Kinachozingatiwa katika khabari mutawaatir ni kutokea kwa yakini kwa khabari hiyo, si kunukuliwa kwa idadi maalum. Kwani mbali na idadi, kuna viashiria vinavyoonyesha nguvu au udhaifu wa Hadith. Khabari inaweza kunukuliwa na idadi fulani ambayo kwa kunukuliwa kwake yakini haitokei, na khabari nyingine inaweza kunukuliwa na idadi inayofanana na hiyo, kisha yakini ikatokea kwa kunukuliwa kwao, kwa kuwa uzingatiaji wa khabari hutofautiana kutokana na tofauti za viashiria, ilhali idadi ni sawa. Kwa hiyo, Hadith mutawaatir ambayo kwayo yakini hutokea ni lazima inukuliwe na kundi, si kwa idadi maalum, na idadi ya kundi hilo pamoja na kutengana kwa maeneo yao iwe ya kiwango ambacho haiwezekani kwayo wao kula njama ya kusema uongo. Kinachozingatiwa katika idadi ni kutowezekana kwa kula njama ya uongo kwa idadi hiyo. Hivyo ni lazima Hadith inukuliwe na kundi ambalo idadi yake inafikia kiwango kinachozuia kula njama kwao ya kusema uongo, na kiwango hicho hutofautiana kwa tofauti za wanaonukuu, hali, na viashiria.